Tumaini La Vizazi Vyote
DIBAJI
Katika mioyo ya watu wote, wa rangi au tabaka zote za maisha, kuna shauku kubwa ya kupata kile ambacho mtu hana kwa sasa. Tamaa hii imewekwa ndani ya mwanadamu na Mungu mwenye rehema, ili mwanadamu asiridhike na maisha yake ya sasa au kutosheka na yale aliyoyapata, yawe mabaya au mazuri au hata bora zaidi. Mungu anataka mwanadamu atafute kilicho bora zaidi na kukipata ili kuibariki nafsi yake kwa baraka za milele.